1 av 6
Moshi baada ya kuwasha mkaa unaotumika kupikia na kadhalika, ukiwa umetanda hewani asubuhi. Picha: Anders Wennersten/SR
2 av 6
Johan Rockström ambaye ni profesa wa sayansi ya mazingira katika chuo kikuu cha Stockholm na mkuu wa kituo cha utafiti cha Stockholm Resilient Center
3 av 6
Idadi ya vyombo vya barabarani vinaongezeka kila kukicha jijini Dar-Es-Salaam. Picha: Anders Wennersten/SR
4 av 6
Dar-Es-Salaam kunajengwa bila ya kusita. Picha: Anders Wennersten/SR
5 av 6
Wanafunzi wakiwa darasani kwenye shule iliyopakana na kituo cha mabasi cha Ubungo.
6 av 6
Punda milia, lakini kwenye picha sio Tanzania,ni mbuga ya wanyama ya kitaifa ya geti la Hell, Kenya. Picha: Pelle Zettersten/SR

Uchumi na idadi ya watu inakuwa kwa kasi kubwa

Idadi ya watu katika bara la Ulaya inakisiwa kupungua kwa asilimia 9 miaka 90 ijayo, China na Urusi watapungua mamilioni ya wakazi. Wakati huo huo, idadi ya watu katika bara la Afrika itaongezeka kwa zaidi ya asilimia 240. Wakazi wa Tanzania mwaka 1950 ilikuwa sawa na idadi ya wakazi wa Sweden, leo wanaishi watu milioni 45 (Sweden ina wakazi milioni 9). Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa, Tanzania inakisiwa kuwa na watu milioni 300 miaka 90 ijayo. Mwandishi wetu Anders Wennersten anatupeleka Tanzania, pale uchumi unakuwa kwa kasi kubwa na wakati huo huo idadi ya watu inazidi kuwa kubwa, mlinganyo mgumu kwa mtizamo wa kusawazisha umasikini na mazingira.

Idadi ya watu katika bara la Ulaya inakisiwa kupungua kwa asilimia 9 miaka 90 ijayo, China na Urusi watapungua mamilioni ya wakazi. Wakati huo huo, idadi ya watu katika bara la Afrika itaongezeka kwa zaidi ya asilimia 240. Wakazi wa Tanzania mwaka 1950 ilikuwa sawa na idadi ya wakazi wa Sweden, leo wanaishi watu milioni 45 (Sweden ina wakazi milioni 9). Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa, Tanzania inakisiwa kuwa na watu milioni 300 miaka 90 ijayo. Mwandishi wetu Anders Wennersten anatupeleka Tanzania, pale uchumi unakuwa kwa kasi kubwa na wakati huo huo idadi ya watu inazidi kuwa kubwa, mlinganyo mgumu kwa mtizamo wa kusawazisha umasikini na mazingira.

Tupo kituo cha mabasi Ubungo, nje kidogo ya jiji la Dar-Es-Salaam lililopakana na bahari ya Hindi. Mabasi yanatifua vumbi jekundu ambalo linatua kwenye mabegi na nguo za wasafiri wanaowasili, kwenye viatu chakavu na hata kwa baadhi ya watu wenye mategemeo na wenye matumaini yasio na kipimo.

Jiji linawapokea kwa nguvu kali na ushupavu mamia ya watu wanaohamia Dar-Es-Salaam – kila siku. Ukuwaji wa mji unaonekana wazi pale msongamano wa mabasi yanapopishana kupitia kituo hiki kikubwa cha mabasi ambacho ni moyo wa watafuta riziki.

Watu hawa wanawasili kutoka mikoani kwenye makabila zaidi ya mia moja, wakikuyu, wasukuma, waluo. Baadhi wakiwa wamevaa nguo zao za tamaduni, wakiwa na mafurushi, vyombo na mablanketi wanaendelea kwenye msongamano. Wengi wao wanakuja na ndoto kubwa za kufanikiwa – kujiimarisha jijini. Wawe ni miongoni mwa ile jamii ya kisasa. Waje kumiliki chumba kwenye moja ya maghorofa mapya. Wanunue chakula kwenye duka kuu la kujihudumia (supermarket). Labda pia kuweza kuwapeleka watoto wao shule iliyopakana na kituo cha basi.

Uchumi wa Tanzania, kama nchi nyingi zao za Afrika Mashariki, umekuwa ukiongezeka kwa asilimia 6-7 katika kipindi chote cha miaka ya 2000. Uchimbuaji wa madini unakua kwa kasi. Sekta za huduma kama vile utalii pia inakua kwa kasi. Nchi ipo katika safu ya juu ya ukuwaji wa kiuchumi barani kupitia pirika zake za kawaida za biashara. Baina ya China na Afrika tu, biashara imeongezeka zaidi ya mara kumi kwenye miaka kumi. Mwaka 2011, biashara baina ya nchi hizi mbili ilikuwa dola za kimarekani bilioni 127. Mfumko wa bei umedhibitwa, mageuzi ya benki yametekelezwa, migogoro imepungua. Ila kinachoongezeka pia ni idadi ya watu barani Afrika, kama masihara. Watu milioni 200 wameongezeka zaidi miaka 10 ya mwisho. Idadi sawa na jumla ya wakazi wa Uingereza, Ujerumani na Ufaransa. Madaraja ya kati na madaraja ya matumizi  yanaongezeka. Na pia idadi ya walala hoi inongezeka. Bila ya kusema kama njozi ya kuwatoa wakazi wote kutoka kwenye dimbwi la umasikini ni changamoto kubwa.

- Mimi ni mmoja wao wanaoishi kule chini, anasema Amiri, ana miaka 49.

Ananyoosha kidole kuelekea kwenye ufukwe uliojaa mafuta na takataka chini ya mti karibia na kivuko cha boti zinazoelekea kwenye furaha kuu ya watalii – Zanzibar. Hawasikii wasafiri wanaowasili. Anadhani ni miaka 15 sasa imetimu tokea alipoiwacha familiya yake na kupanda basi zaidi ya masaa saba mpaka kufika jijini kutokea kijijini, ila mpaka hivi sasa anaishi bila ya kazi, wala makazi. Familiya yake, mkewe na mwanawe Mariamu ambaye anadhani ana miaka 25, hajaonana nao miaka 13 sasa kutokana na hali duni ya kifedha, aliendelea kusema. Labda pia anaona haya kidogo kwa kutofanikiwa kama alivyotegemea.

- Sijui kama mke wangu ameolewa tena au vipi, anasema Amiri. Tunalala watu wengi pamoja ufukweni, waokota chupa na omba omba. Tunajitahidi kulindana kwani tunavamiwa na vibaka mara nyingine.

Kwa upande wa pili wa barabara kutoka kambi ya usiku ya Amiri kuna mabenki na ofisi za biashara kubwa zinazokuwa kwa kasi. Ukuaji wa uchumi na ukuaji wa wakazi unakimbizana kama paka na panya, wakati mmoja wao kwa kiasi kikubwa anamtegemea mwenziwe. Ndani ya mtungi wa ukuwaji wa uchumi kuna mazingira.

Hassan, miaka 28, amenipakia kwenye pikipiki yake kunipeleka eneo mojawapo la walalahoi liliopo kando kidogo ya jiji. Kwa juu panaonekana kama ni duara la mabati yenye kungara kuzunguka kitovu cha mji. Eneo hili lilikuwa ni msitu mtupu miaka kumi iliyopita. Leo hii pamejengwa na nyumba sahili za saruji ambazo hazijapakwa rangi.

- Hapa hapakuwa na njia, hapakuwa na gari wala daladala, anasimulia Hassan. Palikuwa na vijia vyenye mawe hapa baina ya miti. Mtu alikuwa analizimika kutembea kipande kirefu kwenda barabara kuu.

Yule mwenye kuchukua basi kutoka jijini kuelekea upande mwengine wa bara, anaweza baada ya saa kadhaa kufika kwenye zile mbuga za ajabu  na za heshima ulimwenguni; Serengeti, Ngorongoro na Ziwa Manyara. Ziwa Manyara ni pepo ya zaidi ya jamii 400 za ndege. Serengeti kuna mamilioni ya nyumbu, punda milia na swala. Ila shinikizo la ardhi ndani na nje ya mbuga, pale wanyama wa mwituni wanapotembelea sehemu kubwa imeshaanza kupungua na itazidi kupungua endapo idadi ya watu itakaribia kuwa sawa na utabiri wa Umoja wa Mataifa. Lakini kuna ardhi kubwa ya kuchukua anamaanisha mchumi Francis Matambalya ambaye ni mtaalamu wa biashara za kimataifa, kutoka Tanzania anayefanya kazi Taasisi ya Kinodiki ya Afrika iliyopo Uppsala.

- Afrika, sehemu ya pili kwa ukubwa baada ya Asia, sio watu wengi sana wanaoishi mijini, idadi ya watu wanaoishi kwenye nchi zake 50 haijafikia idadi ya wakazi wa India ambapo kwa ukubwa wake ni sehemu moja ya kumi tu ya Afrika. Kuna ardhi ya kutosha ya kuchukua na kuotesha mazao, anaendelea kusema Matmbalya baada ya kuulizwa kama Tanzania ni nchi ya watu tu sio ya swala na nyumbu pia. Nyinyi wazungu mliua wanyama pori wenu kwa sehemu kubwa, wamarekani waliua karibia baisani (aina ya nyati) wote. Na kuhusu shinikizo la ardhi kupitia ukuwaji wa idadi ya watu, inaweza kupungua kwa kukuwa kwa miji, yaani watu wengi zaidi kuhamia mijini.

Mara zote ukuaji wa miji na kuongezeka idadi ya watu imekua ni vigezo vya ukuaji wa uchumi, anasema mchumi Francis Matambalya. Wakati wakosoaji wa ukuaji wa miji labda wangeweza kugeuza kuwa mtu anahitaji uwezo zaidi kwenye mfumo wa maisha wa matumizi mijini kuliko kwenye mfumo wa maisha wa vijijini.

Ukuaji wa miji ni njia ya kupunguza umasikini. Na Afrika, bara ambalo ukuaji wake wa mijini ni mdogo duniani, maendeleo yake hayapo nyuma kwa kuongezeka idadi ya watu anamaanisha Matambalya, “bali rasilimali tulizonazo hatuzitumii ipasavyo, zinawanufaisha wengine”, anasema Matambalya.

- Tatizo moja ni kuwa washirika wa biashara za kimataifa wanakuwa sio wafanyabiashara wa sehemu husika, bali ni wanasiasa wa sehemu husika, ambapo inafungua milango ya rushwa. Miaka 500 sasa hali hii inaendelea – kama ni njia panda ya Afrika. Sisi watanzania hatuna ujuzi wa kupatana hivyo watu wa Magharibi wanafaidika. Hilo ndio tatizo, bila ya kujali  idadi ya watu, anamaanisha Matambalya.

Tunarudi kwenye maeneo ya walala hoi, kunakuja wanaharusi… watu wapatao 50 wanacheza kuzunguka mdundo mkali wa muziki, maharusi wakiwa ni kipaumbele na wakiwa na hisia za matumaini ya siku zijazo katikati ya usahili. Ikiwa huyu bi harusi mwenye kutabasamu hapa Dar-Es-Salaam kwenye majengo ya usahili atafuata nyayo za uzazi wa wastani kwa watanzania, atakuja kuwa na watoto wapatao watano. Laiti angeishi kijijini basi angeweza kuja kuwa na watoto mpaka sita kwa saba.

Wakati idadi ya watu Ulaya mpaka ifikapo mwaka 2100 itapungua kwa asilimia 9, na Asia watakuja kuongezeka kwa wastani huo, Afrika watakuja kuongezeka kwa kipindi hicho cha miaka 90 ijayo kwa asilimia 240. Yote haya kwa mujibu wa utabiri wa Umoja wa Mataifa. Kama sehemu nyengine ulimwenguni, watu wanazeeka, lakini pia – tofauti na sehemu nyengine ulimwenguni – kutokana na kuendelea kuwa na watoto wengi. Jukumu lake kama mama katika familiya kubwa ijayo linajumuisha mripuko wa idadi ya watu ni changamoto za kipekee.

Katika mkutano mkubwa wa wanawake kwenye hoteli nzuri mojawapo iliyopo mjini anashiriki Halima Shariff kutoka kwenye mtandao wa viongozi wanawake wa Afrika. Anataarifu kuhusu idadi kubwa ya wanawake wanaofariki kwa uzazi kila mwaka kutokana na upungufu wa huduma za afya kwa wajawazito na wazazi. Kuhusu vifo kutokana na utoaji wa mimba. Na pia kuhusu mchango wa wanawake katika maendeleo ya uchumi yanahitaji kutambuliwa na kupimwa. Kwa kuwaboresha sio kwa kuwaweka kando.

- Hivi sasa ambapo nchi inakuwa kwa kasi, wanawake hawashiriki kikamilifu katika mazungumzo ya umma, si masuala ya kiuchumi, ya kijamii wala ya siasa, anasema Halima.

Kwa kushajiisha nafasi ya wanawake ni muhimu kujadili japo kama kwa kiasi fulani ni mwiko…uzazi wa mpango. Kitu ambacho sio zamani sana kilidhaniwa na baadhi ya watu kuwa ni ubunifu wa watu wa magharibu (watu weupe) kutaka kuwaingilia na kuwapangia waafrika haki yao ya kupata watoto, lakini bado ni suala la utata.

- Kiutaalamu ninahamu ya kusema kuwa ingekuwa vyema na uzazi mdogo, anasema Halima Shariff. Ingeweza kuupa uchumi nafasi ya kutosheleza watu.  Kwa mfano, Serikali ingeweza kuekeza zaidi kwenye elimu na afya, maendeleo ya watu kuwa ya ubora kuliko ya uwingi. Lakini kiutamaduni ni tofauti. Hakuna, bila ya kuwaacha wanasiasa, wanaotaka kuzungumzia kuzaa watoto wachache. Haipo hata katika ajenda. Badala yake tunazungumzia uwezekano wa uzazi wa mpango ili watoto angalau wapishane baina ya miaka 2-3 kwa ajili ya kuboresha uwezekano wao kwenda shule.

Lakini suala hili si rahisi. Utamaduni unaelekea upande mmoja, na uchumi unaelekea upande mwengine. Utamaduni unabadilika taratibu wakati uchumi unakua haraka. Uchumi wa China unakua, juu ya siasa ya mtoto mmoja. Lakini sisi hatutaki, hatuwezi kuchukua hatua kali kama hiyo – kutokana na sababu za kitamaduni, anasema Halima Shariff.

Changamoto nyingi, elimu, mfumo wa hifadhi ya jamii na huduma za afya kwa wagonjwa. Idadi ya watu ulimwenguni inazidi kuongezeka – lakini kwa kiasi kikubwa kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu Afrika. Baada ya miaka 90 tutakuwa watu wapatao bilioni 3 zaidi duniani kulinganisha na hivi leo. Ni zaidi ya watu wote waishio Ulaya, Afrika, Marekani ya Kaskazini na Marekani ya Kusini kwa pamoja. Na muda huo huo – juu ya yote – idadi ya watu China itapungua katika kipindi hicho, miaka 90 ijayo, kwa milioni 400. Sehemu zote mbili yafaa kutumia kipindi hicho kiuhalisi kwani idadi ya nguvukazi inaongezeka na idadi ya wazee na watoto inapungua. Yote ni kwasababu wakazi wa nchi wawahi kutajirika kabla hawajezeeka. Hayo anasema mtaalamu wa Afrika na mchumi Peter Stein.

Demografia ni muhimu katika ukuwaji wa kiuchumi, kwa kawaida inakuwa inazungumziwa kuhusu “demographic divident”, inakuwa inatokezea katika nchi ambayo idadi ya nguvukazi wao inaongezeka kwa gharama ya wazee na watoto, kwani wazee na wadogo ndio wafaidi halisi. Ni maelezo muhimu ya kwanini uchumi wa nchi za kiasia ulikuwa kwa nguvu baina ya mwaka 1960-1990, kwa kiwango ambacho nchi chache za Afrika zimefikia kwani bado watoto wanazaliwa kwa wingi na watoto wadogo ni sehemu kubwa ya idadi kamili ya watu. Kwa maana nyengine, Afrika bado inasafari kubwa kabla ya kufikia “the demographic divident”. Hata hivyo miaka kumi iliyopita inaonyesha kuwa Afrika haijabanwa kwenye mtego wa umasikini, inahusu Afrika kama nchi nyengine duniani kutengeneza mfumo wa kiuchumi wenye kufungua milango ya biashara za kimataifa na biashara ili kuendelea kukua kiuchumi. Endapo waafrika wataendelea kufanya mageuzi kwenye uchumi wake, wataendelea kukua kiuchumi na hata hapo mbeleni wataweza kufaidi “the demographic divident”, anasema mchumi Peter Stein.

Hivyo ndivyo vinavyokuwa bega kwa bega, ukuwaji wa uchumi kama idadi ya watu. Na changamoto nyingi za kijamii na za kisiasa wakati mamia ya mamilioni ya wakazi wapya katika karne zijazo itaongezeka, kwa Tanzania tu watahitaji kuwa ni sehemu ya ukuwaji wa mfumo wa hifadhi ya jamii, huduma za afya na elimu. Na kuwa na mamilioni kwenye mfuko wakati ujenzi wa barabara mpya, maeneo ya makazi na uchimbaji wa mafuta na gesi utakaposhamiri.

Ulimwenguni watu kama bilioni tatu zaidi wataongezeka kwenye mtindo wa kimagharibi wa kukukua kiuchumi ambao jadi yake unajenga katika kuongeza mahitaji ya malighafi kwa watu wanaoendelea kuongezeka. Lakini kwa kidemografia inavyoonekana haileti uwiano mzuri duniani ikiwa idadi ya watu wanaopungua hivi sasa au miongo ijayo kwenye nchi kama China, Urusi, Japan na Brazil, idadi ya wakazi kusimama kama ilivyo Ulaya na mfumko wa idadi ya watu katika sehemu kubwa ya Afrika. Itakuwa ni vigumu kutatua mchanganuo huo.  Ulimwenguni idadi ya watoto wanaozaliwa kwa mwaka haiongezeki, hii ikiwa ni mwanzo wa mwisho wa kukua kiuchumi. Lakini uzazi Afrika unaenda kwa hatua kubwa kinyume na mfumo huu. Wanawake Tanzania wanajifungua wastani wa watoto 6 bado, vivyo hivyo Nigeria, Kongo, Kinshasa, Burkina Faso, Zambia, Somalia na Malawi. Kenya na Liberia ni wastani wa watoto watano kwa mwanamke. Niger ni watoto 7. Ikiwa watoto wanne wataendelea kuishi katika kila familiya basi idadi ya watu itaongezeka mara mbili kwa kila kizazi.

Kwa mtazamo wa kimazingira, ukuaji wa kiuchumi na idadi ya watu unatupa ishara muhimu ya kuwajibika kwa nchi za magharibi. Hivyo anasema Johan Rockström ambaye ni profesa wa sayansi ya mazingira katika chuo kikuu cha Stockholm na mkuu wa kituo cha utafiti cha Stockholm Resilient Center.

- Kwa mwendo huu ambao mataifa masikini wanahitaji kutumia sehemu zaidi kwa kutoa “green house gases”, kutumia ardhi, maji, metali nk ndipo lazima mataifa kama Sweden na mengineyo yaliyoendelea yajirekebisha haraka zaidi ili kutayarisha njia na nafasi kwa maendeleo tunayoyaona katika mataifa masikini. Inahusu usawazishaji na siasa ya kugawana ulimwenguni katika kile kilichobaki kuhusiana na mazingira hapa duniani. Sayansi inatuonyesha wazi kuwa tunahitaji kujirekebisha tusiwe tegemezi wa mafuta ya kisukuku kwenye uchumi wa dunia miaka 40 ijayo, kitaalamu inawezekana na huenda pia ikahitajika kufanya hivyo katika mtazamo wa kiuchumi. Hivyo, hii ni nafasi ya kipekee kwa nchi zenye kukua haraka kiuchumi wasije wakaganda katika teknolojia ya zamani. Badala yake wanaweza kwenda moja kwa moja kwenye mawasiliano ya simu za mikononi, usafiri wa umma wa kisasa, kutumia mbinu endelevu ya kuzalisha chakula na zaidi ya yote kwenda kwenye utumiaji wa nishati mbadala.

- Kwa hizi mbinu mpya na za kisasa zinazoweza kutumika, unaona ishara gani kuwa zinatumika Afrika?

- Ishara ni ndogo Afrika, hususan inapohusiana na ukuwaji wa miji. Mengi zaidi yanaweza kufanyika kwa kupanga miji ili iweze kutosheleza matakwa ya mazingira ya maisha ya mjini. Hivi sasa miji inakuwa haraka bila ya kudhibitika. Juu ya kujitegemea chakula, hatua mbalimbali zinachukuliwa zaidi. Kwa mfano Ethiopia kuna mradi wa kitaifa wa kilimo endelevu. Nchi kama Tanzania ina kila fursa ya kuweza kuekeza  vyema kwa mtazamo wa muda mfupi na muda mrefu. Mbali na vitu vyengine, inahusiana na uzalishaji wa nishati ya mimea inayotokana na ethanoli ya mua ambayo inafaa sana, mradi ambao Sweden na Tanzania wanashirikiana hivi sasa. Na pia mradi mkubwa wa kutumia nguvu za jua, upepo  na kukamilisha mzunguko wa mbolea kutoka mijini kwenda vijijini, ninamaanisha kurudisha mkojo na kinyesi katika eneo kubwa lenye kukamilisha mfumo wa mzunguko. Kitu ambacho tunapata shida sana kufanya katika miji iliyokuwa mikubwa, lakini Tanzania, Kenya, Zambia, Uganda na Ethiopia wana fursa isiyo na kipimo. Kama watafanikiwa, siwezi kusema. Kuhusu sekta ya nishati, nishati ya kisukuku ndio ambayo ya haraka, rahisi na ufumbuzi wa muda mfupi na hapa panahitajika kuwaza mbele zaidi. Hivyo, kuna kazi kubwa ya kufanya,  anasema Johan Rockström.

Labda ufumbuzi ni kama watu wengi wangekuwa na mawazo kama ya Joshua, kijana wa miaka 30 aliyekaa mgahawani na kusema jinsi hali ilivyo nzuri hivi sasa barani Afrika. Angalau mbali ya watu wengine, juu yake yeye binafsi.

- Hapa hamna migogoro ya kifedha, hapa sisi tunaishi kindugu, maisha yanaenda mbele, anasema Joshua ambapo yeye mwenyewe amerudi Tanzania baada ya kumaliza miaka sita ya masomo yake Uingereza.

- Hatuhitaji magari ya fahari yanayomlazimu mtu kufanya kazi kupita kiasi kwa ajili ya kuwa na uwezo nayo. Kitu mnachopenda Ulaya ni kazi na bia. Kiwango changu, ambacho kipo chini sana kuliko familia ya daraja la kati la mswidi, ni zaidi ya kunitosha. Sisi waafrika hivi sasa ndio watu wenye furaha kuliko wote duniani, anasema Joshua.

Mwandishi Anders Wennersten
klotet@sr.se

Imetafsiriwa na Asya Uhlås (översättning till swahili: Asya Uhlås)

Grunden i vår journalistik är trovärdighet och opartiskhet. Sveriges Radio är oberoende i förhållande till politiska, religiösa, ekonomiska, offentliga och privata särintressen.
Du hittar dina sparade avsnitt i menyn under "Min lista".